Na Lulu Mussa ,Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Ummy Mwalimu ameahidi kutoa mafunzo ya pamoja kati ya Wabunge, Wakurugenzi na Viongozi wa Halmashauri kwa upande wa Zanzibar ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu usimamizi wa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo.

Amebainishwa hayo hii leo katika kikao kazi kilichofanyika katika Ukumbi wa Msekwa Jijini Dodoma, baina ya wabunge wa Zanzibar na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa lengo la kujadili namna bora katika kufanikisha utekelezaji wa fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo.

Amesema kumekuwa na changamoto katika kuratibu fedha za kuchochea maendeleo ya Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar na kuwahakikishia wabunge kuwa Ofisi yake itaangalia namna bora katika kufanya marekebisho ya Sheria ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza.

“Nimesikiliza changamoto zilizoainishwa naahidi kuwasilisha mapendekezo ya kufanya marekebisho ya mfuko wa kuchochea Maendeleo ya Jimbo na kuratibu mafunzo ya pamoja ili wananchi wetu waweze kunufaika na fedha zinazotolewa kwa ufanisi na wakati” Ummy alisisitiza.

Pia, Waziri Ummy amewahakikishia wabunge hao ushirikiano katika kuratibu masuala ya Muungano na yale yasiyo ya Muungano.

Kwa upande mwingine mmoja ya Wabunge kutoka Zanzibar Mhe. Ali Hassan Omary (King) kutoka Jimbo la Jang’ombe amesema Mabadiliko ya Sheria kuhusu Mfuko wa kuchochea maendeleo ya Jimbo na kikao baina ya Watendaji wa Halmashauri na Wabunge wa Zanzibar vitatoa suluhu kwa changamoto zilizopo hivi sasa.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Joseph Malongo amesema kikao hicho kimekuwa cha manufaa na hazina kubwa sana katika kuratibu masuala ya Muungano.

“Kwa kuwa Sheria hii ya kuchochea maendeleo ya Mfuko wa Jimbo imekuwa ya muda mrefu toka mwaka 2009, wataalamu watakaa ili kuangalia kama iko haja ya kutengeneza kanuni pia tutapeleka mapendekezo kwa wenzetu wa TAMISEMI ili iweze kufanyiwa marekebisho” Mhandisi Malongo alisisitiza.

Katika kikao hicho mada tatu zimewasilishwa ikiwa ni pamoja na Sheria ya Mfuko wa Jimbo, Usimamizi na Utekelezaji wa Fedha za Mfuko wa Jimbo na Changamoto za Mfuko wa Jimbo Zanzibar na Maoni ya kukabiliana nazo.