Tume ya watu saba iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kuchunguza kifo cha dereva wa lori aliyefahamika kwa jina la Abdulhman Issa imebaini kuwa dereva huyo alifariki kutokana na changamoto ya kushindwa kupumua.


Akizungumza na wandishi habari ofisini kwake RC Chalamila amesema dereva huyo alishikiliwa na jeshi la polisi katika eneo la Shamwengo wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya akiwa anaendesha gari lililokuwa likimshinda kutokana na tatizo alilokuwa nalo.

Chalamila amesema aliunda tume baada ya kuwepo kwa taarifa za mkanganyiko kuhusu kifo cha dereva huyo, na tume aliyoiunda imefanya uchunguzi wa kina kwa muda wa siku tatu na kubaini kuwa dereva huyo alipatwa na maradhi ya mfumo wa upumuaji akiwa katika Hospital ya Chimala iliyopo Wilaya ya Mbarali.

Aidha, ripoti inaeleza tayari madaktari bingwa wamefanya uchunguzi wa kina ikiwa pamoja na kufanya upasuaji wa maiti hiyo na kubaini marehemu hakuwa na jeraha lolote la kupigwa na askari.

Sitofahamu iliibuka hivi karibuni baada ya kusambaa kwa picha zikionesha dereva huyo akishushwa na polisi kutoka kwenye gari alilokuwa akiendesha.