Na Prisca Ulomi, WMTH
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile ameuelekeza uongozi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa 27 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania lililofanyika Dodoma.  Amefafanua kuwa hivi sasa dunia ipo kiganjani na inatumia TEHAMA na maisha yanakwenda kidijitali hivyo TPC nayo iongeze matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kuhudumia wateja kwa kuwa kwa kufanya hivyo TEHAMA itaongeza mapato ya Shirika na kuongeza gawio lake kwa Serikali.

“Sitarajii kuona TPC inaendeshwa kwa hasara, tumieni rasilimali za Shirika kwa ajili ya ustawi wa Shirika na sio ustawi wa mtu binafsi”, amesisitiza Dkt. Ndugulile.

Aidha, amepongeza TPC kwa utendaji kazi wao na ametaka mfanyakazi mmoja mmoja wa TPC kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kila kiongozi wa Shirika kusimamia vizuri eneo lake la kazi na kutekeleza majukumu yake.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Baraza ni chombo muhimu sana maeneo ya kazi na lipo kisheria na kwa hali ninayoiona hapa inaonekana kweli amani imetawala na kuna ushirikiano baina ya wafanyakazi na viongozi wa TPC na naamini kwa uongozi wako kwenye Wizara hii mpya tutahakikisha TPC inasimama imara katika kuhudumia wateja kwa kuwa tuna kiu ya kuona Shirika hili linakimbia.

Naye Postmasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe amesema kuwa wajumbe wa Baraza hilo watakuwa na kikao cha siku tatu ambapo watajadili mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Shirika kwa mwaka 2021/2022; matumizi ya mifumo mipya ya kidigitali kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kila siku; sheria ya utumishi wa umma, wajibu na haki za kila mfanyakazi na kujadili maslahi ya wafanyakazi; mahusiano mahala pa kazi; na nidhamu katika utendaji kazi.

Kikao hicho kimejumuisha Menejimenti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo; Dkt. Jim Yonazi; Mameneja wa TPC wa Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na viongozi wa vyama vya Wafanyakazi wa Shirika hilo.