Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezipiga faini ya zaidi ya Sh.Bilioni 38 Kampuni Sita za Simu za Mkononi kutokana changamoto za utoaji huduma za mawasiliano.
Akizungumza na waandishi Habari Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi James Kilaba amesema kuwa faini hizo zimetokana baada ya TCRA kupima Ubora wa huduma za mawasiliano ya simu za Mkononi na kubaini kuwa na changamoto katika maeneo 11 walizopima.
Amesema fedha hizo za faini wanatakiwa waziweke katika akaunti zao kwa ajili ya kuboresha huduma za mawasiliano ndani ya miezi mitatu.
Mhandisi Kilaba amesema upimaji wa huduma za mawasilio kwa kampuni sita za simu za Mkononi ulifanyika katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Kilimanjaro, Mbeya, Unguja, Tanga pamoja na Simiyu kwa kuangalia vigezo mballimbali.
Ametaja faini kwa kila kampuni ambapo Airtel Tanzania Plc sh.bilioni 11,519,775,721.58, MIC Tanzania Plc Tigo sh.Bilioni 13,032,049,305.32,Viatel Tanzania Plc Hallotel sh. bilioni 3,409,107,801,.61,Vodacom Tanzania Plc Sh. bilioni 7,810,714,298.68,Zanziabar Telecom Plc ZANTEL Sh. bilioni 1,021,407,142.89 pamoja na TTCL Corperation Sh. bilion 1,336,266,570.42.
Aidha maeneo waliyopima ni kiwango cha simu zilizoshindikana kuunganishwa, kiwango cha simu zilizo katika muda wa kuunganisha simu iliyopigwa, wigo wa upatikanaji wa huduma, kiwango cha simu zilizofanikiwa kuunganishwa, kiwango cha uwezo wa minara kupokezana mawasiliano, wastani wa muda unaotumika katika kupakia na kupakua data, uwiano wa muunganisho wa data, pamoja na Upatikanaji wa huduma za jumbe Fupi.
Amesema kwa mujibu wa kanuni ya 20 ya kanuni hizo mtoa huduma atakayeshindwa kufikia vigezo vya ubora wa huduma anawajibika kulipa faini za viwango mbalimbali.
Amesema kuwa kutokana na faini hiyo kila mtoa huduma anatakiwa kuwasilisha mpango kazi kimaandishi TCRA ndani ya Siku tatu wa namna atakavyotumia fedha hiyo ya faini katika kuboresha huduma zake kama alivyoelekezwa.
Hata hivyo amesema mtoa huduma yeyote atashindwa, atakataa au kupuuza maagizo hayo TCRA itachukua hatua kali zaidi za kiudhibiti na kisheria pasipo kutoa taarifa zaidi kwa mtoa huduma.
TCRA itafatilia matumizi ya fedha namna zinavyotumika katika kuboresha huduma ya mawasiliano kwa simu za mkononi.