Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeiruhusu Wasafi TV kurusha matangazo kuanzia Machi 1, 2021, baada ya kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na kituo hicho kikiomba kupunguziwa adhabu ya kufungiwa kwa miezi sita.

Kwa siku tofauti, Wasafi TV iliwasilisha utetezi wao TCRA, ikiwa ni pamoja na kukiri kurusha matangazo mbashara kinyume na masharti na leseni, huku ikiomba adhabu hiyo kupunguzwa.

Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba imeeleza kuwa baada ya kusikiliza wasilisho la Wasafi TV, mamlaka hiyo imetafakari upya uamuzi wake na kutaja masharti matatu ya kufuatwa na kituo hicho ikiwemo kuendelea kutumikia adhabu hiyo mpaka Februari 28, 2021.

Pia, kituo hicho cha televisheni kimetakiwa kuzingatia masharti ya leseni ya kutoa huduma za maudhui ya kulipia kwa njia ya televisheni na iwapo kitashindwa, kitakataa au kukaidi uamuzi huo, hatua zaidi za kisheria na kiudhibiti zitachukuliwa dhidi yao.

Januari 5, 2021 TCRA ilikifungia kituo hicho kwa kipindi cha miezi sita kwa kukiuka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji wa Redio na Televisheni), 2018.