Tanzania imechaguliwa kunufaika na mradi wa Euro milioni 3 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 8 kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani wa samaki aina ya migebuka na dagaa kutoka ziwa Tanganyika.

Mradi huo utatekelezwa Mkoani Kigoma kwa kipindi cha miaka mitano na kusimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) ambapo wavuvi wadogo watapatiwa ujuzi wa kuongeza uzalishaji,kusaidia kupunguza upotevu wa mazao ya samaki,kuyawezesha mazao ya samaki kufika kirahisi katika masoko ya ndani na ya Kimataifa pamoja na utunzaji wa mazingira ili kuwezesha uvuvi endelevu na wenye tija.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 kati ya 79 za Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (OACPS) zilizochaguliwa kutekeleza mradi huo unaojulikana kama Fish4ACP utakaotekelezwa kwa gharama ya Euro milioni 40 kupitia mfuko maalum wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EDF11 for Intra – ACP Projects) nchi nyingine ni Cameroon, Ivory Coast, Nigeria, Sao Tome, Senegal na Zimbabwe kwa upande wa Afrika,Jamhuri ya Dominica, Guyana na Visiwa vya Marshall kwa upande wa Caribbean na Pacific

Kupatikana kwa mradi huu ni utekelezaji wa wa agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli wakati akizindua Bunge la 12 na kuielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Balozi za Tanzania nje ya Nchi kuhakikisha sekta ya uvuvi inatoa mchango kwenye kukuza pato la Taifa,kukuza ajira na kupambana na umasikini.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ubalozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji imeomba kibali kutoka Umoja wa Ulaya kuruhusu dagaa wa Kigoma kuuzwa katika soko la Ulaya ambapo tayari kampuni moja ya Kitanzania imekwishaingia makubaliano ya kuuza tani 20 za dagaa hao kila mwezi nchini Ubelgiji na upatikanaji wa kibali ukikamilika dagaa wa Kigoma watauzwa kwa wingi katika nchi mbalimbali za Ulaya kama ilivyo kwa minofu ya sangara.