Na Mwandishi Wetu
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja Jamhuri ya Afrika Kusini zimewasilisha ombi maalumu kwa Umoja wa Afrika kuzitambua rasmi njia zilizotumika na wapigania uhuru kutoka Dar es Salaam kupitia nchi mbalimbali Kusini Mwa Bara la Afrika hadi Namibia kuwa urithi wa Kimataifa.

Ombi hilo limewasilishwa na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa katika Mkutano wa 34 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika kwa njia mtandao na kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ambaye alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.  

Tanzania pia imeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni Sanaa, Utamaduni na urithi.

“Tumeuomba Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili na ya ukombozi katika Bara la Afrika kwa kuwa ndiyo lugha iliyotumika kwa ajili ya mawasiliano na mafunzo kwa wapigania uhuru ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni sanaa, utamaduni na urithi,” Amesema Prof. Kabudi.

Akiufunga Mkutano huo wa siku mbili, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Felix Tshisekedi amesisitiza kuwa umoja, mshikamano na amani katika bara la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakayoliwezesha bara hilo kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali ilizonazo.

“Umoja, mshikamano na amani katika bara la letu la Afrika ndiyo nyenzo pekee itakatuwezesha sisi kuendelea kiuchumi ili kuendana na rasilimali tulizonazo kwa maslahi yetu mapana,” Amesema Rais Tshisekedi

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umejadili mambo mbalimbali ikiwemo uundaji wa Kamati mpya ya uongozi wa Umoja wa Afrika (the AU Bureau of Assembly) kwa mwaka 2021, uzinduzi wa Kaulimbiu ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2021 inayohusu “Sanaa, Tamaduni na Urithi katika kufikia azma ya Afrika Tuitakayo”

Mengine yaliyojadiliwa ni taarifa ya Maendeleo ya Mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu COVID-19 Barani Afrika, taarifa ya Utekelezaji wa Mabadiliko ya Kitaasisi ya Umoja wa Afrika; na Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitumia fursa hiyo kueleza utayari wake kuendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na Nchi Wanachama wa Umoja huo katika kutekeleza jitihada zinazolenga kuiwezesha Afrika kujitegemea.