Na Englibert Kayombo, WAMJW – Dodoma
Taasisi za Sekta ya Afya na Vyuo vya afya nchini vimetakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuboresha tiba asili ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika kupambana na magonja ya kuambukiza na yasiyoambukiza.

Wito huo umetolewa jana na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bw. Edward Mbaga alipokuwa akifungua kikao kazi cha viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya na Vyuo vya taaluma ya afya nchini kilicholenga kuboresha ushirikiano na kuangalia namna ya kuongeza rasilimali katika kuboresha tiba asili nchini.

“Tumekutana hapa ili kuwa pamoja tujadili jinsi ya kushirikiana katika kupata frdha za kugharamia uzalishaji na kufanya tafiti za kutambua usalama, ubora na ufanisi wa dawa za tiba asili nchini” amese Bw. Mbaga wakati akifungua kikao kazi hicho.

Amesema kuwa Jamii imekuwa ikitumia huduma za tiba asili kwa ajili ya kutibu magonjwa mbalimbali na baadhi ya wananchi wanatumia huduma zote mbili kwa maana ya tiba ya kisasa na tiba asili katika kutibu magonjwa.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha utoaji wa huduma hizi kwa kuhakikisha Jamii yetu inaatumia dawa salama, yenye ufanisi na ubora katika kulinda afya ya jamii kwa ujumla, hili linawezekana kwa kufanya tafiti za kina kwa dawa zetu”amesisitiza Bw. Mbaga.

Amesema kuwa Serikali imekwisha tambua tiba asili kuwa na umuhimu toka mwaka 1969 ambapo ilielekeza Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya tafiti za miti dawa ili kuweza kuleta Ushahidi wa kisayansi na kujibu maswali mbalimbali yanayohusu usalama, ubora naufanishi wa dawa za asili ambazo kwa Tanzania kuna zaidi ya miti dawa 12,000 ambayo inatibu magonjwa mbalimbali.

Aidha Bw. Mbaga amezitaka taasisi zote zinazohusika katika mausala ya tiba asili kushirikiana kwa pamoja ili kuja na majibu yanayoleta tija kwa taifa na kusaidia upatikanaji wa dawa za asili yenye manufaa kwa watanzania na ulimwengu kwa ujumla.

“Taasisi zinafanya taifiti lakini tatizo lililopo hapa ni kwamba kila taasisi inafanay kazi peke yake na kusababisha tafiti nyingi kujirudia rudia, hii inasababisha matumizi ya rasilimali ndogo zilizoppo kutotumika kwa mapana kuweza kufanya tafiti nyingi tofauti na kuleta tija kwa jamii” ameeleza Bw. Mbaga.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa ni lazima viongozi wote wa taasisi na vyo vya afya nchini kuwa na mtazamo chanya juu ya tiba asili kuwa zinaweza kusaidia katika kutibu magonjwa mbalimbali

“Ni muhimu kuunganisha mawazo yetu sisi viongozi na wasomi mbalimbli ili tuweze kuonyesha kwamba sisi wenyewe wasomi tunatambua mchango wa tiba asili katika nchi yetu kwa ajili ya kukinga na kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza” amesema Prof. Makubi

Amesisitiza kusema kuwa dawa zote za asili ni lazima zifanyiwe utafiti kabla ya kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya matumizi na ili kufanikisha hilo ni lazima tuwe na rasilimali za kutoka kuwezesha kufanya tafiti za kina juu ya dawa hizo za asili.

“Mheshimiwa Rais amekwisha toa maelekezo ya bajeti ya afya kuongezwa kwenye upande wa tiba asilia, pamoja na kuunganisha nguvu za Serikali, lakini pia taasisi bado zina uwezo wa kuchangia kuhakikisha tafiti kwa ajili ya tiba asili zinafanyika”Amefafanua Prof. Makubi