Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limefanikiwa kukamata silaha mbalimbali 160 zinazodaiwa kuwa ni haramu katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2020 pamoja na watuhumiwa 68.

Akizungumza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa amelitaja tukio hilo kuwa ni la msimu wa mwaka mzima wa 2020 kufuatia misako iliyokuwa imefanywa na jeshi hilo kwa kushirikiana na kikosi cha dhidi ya ujangili pamoja na pori la akiba la Liparamba chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Kamanda Maigwa amezianisha silaha hizo zilizokamatwa kuwa magobole 149, rifle 3 na shortgun 8 na kuzifanya jumla ya silaha 160 na kuwa msako bado unaendelea wa kuzitafuta silaha nyingine pamoja na watu ambao wamekuwa wakimiliki silaha hizo kinyume na taratibu.

Amesema kuwa licha ya kuzikamata silaha hizo lakini bado jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa 68 ambao wanadaiwa wamekuwa wakizimiliki baadhi ya silaha hizo kinyume na taratibu za kisheria na kuwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi upelelezi ukishakamilika.

Amefafanua kuwa silaha hizo ambazo zilizokuwa zikimilikiwa kinyume na taratibu zingeweza kusababisha madhara kwa jamii ikiwemo na kuzifanyia ujangili wa kuwatekeza wanyama hasa tembo waliyopo kwenye mapori ya hifadhi ya mkoani humo huku amewataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria wazisalimishe haraka kabla ya mkono wa dola haujawafikia.

Kwa upande wake Keneth Sanga, Kamanda wa Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) mkoani humo amesema kuwa silaha hizo zimekamatwa katika maeneo mbalimbali hasa yanayozunguka maeneo ya hifadhi ya wanyamapori ndani ya mkoa huo.

Sanga amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na baadhi ya raia wema kutoa taarifa za uwepo wa watu wanaomiliki silaha hizo kinyume na taratibu na kuwa ameiomba jamii kuendelea kuwa na ushirikaino kama ilivyo kwenye jumuiya mbalimbali zilizoundwa kwa ajili ya kulinda maeneo ya mapitio ya wanyama (USHOROBA).