Na Faraja Mpina- WMTH
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt Zainab Chaula amelitaka Shirika la Posta Tanzania (TPC) kujitathmini juu ya utekelezaji wa malengo waliyojiwekea katika kipindi hiki cha kuelekea robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2020/2021.

Dkt Chaula aliyazungumza hayo wakati akifunga Mkutano wa Baraza la 27 la Shirika hilo lililofanyika jijini Dodoma la kujadili na kutathmini juu ya utendaji kazi wa Shirika hilo

Ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha mwaka ni matarajio Shirika hilo kufikia asilimia 60 ya malengo waliyojiwekea, na kama halijafikia asilimia hizo Shirika linatakiwa kujitathimini na kuelekeza nguvu katika mikoa ambayo haikufanya vizuri ili  kuiwezesha nayo iweze kwenda sambamba na matarajio ya Shirika hilo.

Dkt Chaula ameongeza kuwa Shirika la Posta limepata watendaji wabobezi kitaaluma, wabunifu, waadilifu na wenye maadili ya utumishi wa umma ambao wanatakiwa kuwasaidia viongozi wao kwa maendeleo ya Shirika

“Hakuna kiongozi ambaye hawezi iwapo akisaidiwa na watendaji wake, ukiona kiongozi hafai maana yake watendaji anaowaongoza hawamsaidii, hawamshauri na hawatizimi wajibu wao katika utendaji”, Dkt Chaula

Aidha amesisitiza upendo, amani na mshikamano mahali pa kazi kuepusha malumbano na manung’uniko ili kuimarisha utendaji kazi wa Shirika hilo.

Naye Dkt Jim Yonazi Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo amempongeza Postamasta Mkuu Hassan Mwang’ombe na watendaji wake kwa kufanya biashara ya ushindani na kuleta matokeo yanayoonekana na kuwaasa watendaji wa Shirika hilo kuendelea kushikamana kwa kufanya kazi kwa juhudi na kujituma.

Awali Postamasta Mkuu Mwang’ombe akitoa taarifa kabla ya kufungwa kwa Mkutano wa Baraza hilo alisema watendaji wa Shirika wamepata  mafunzo mbalimbali kupitia Baraza hilo ikiwemo mafunzo ya kuvitambua viashiria hatarishi kwa uendeshaji wa Shirika, namna ya kuviepuka na kuvitatua viashiria hivyo.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari