Shirika la Afya Duniani, WHO limesema kwamba idadi ya visa vipya vya virusi vya corona vimepungua kwa asilimia 16 ulimwenguni wiki iliyopita. WHO imesema kuwa takwimu hizo zimepungua kwa visa 500,000 hadi milioni 2.7. 

Wiki ya kwanza ya Januari, visa vipya vya corona viliongezeka kwa takriban milioni 5. Wiki iliyopita karibu maeneo yote ulimwenguni yalishuhudia kupungua kwa maambukizi ya COVID-19, isipokuwa katika eneo la Mashariki ya Kati. 

Pia idadi ya vifo vilipungua duniani wiki iliyopita, kwa vifo vipya 81,000, ambapo vimepungua kwa asilimia 10. Kupungua kwa maambukizi ya virusi vya corona pamoja na vifo kunatokea wakati ambapo nchi nyingi zinaendelea kutoa chanjo. 

Wakati huo huo, Afrika Kusini imeahidi kutoa dozi milioni moja za chanjo ya AstraZeneca kwa mataifa mengine ya Afrika na nchi hiyo imeamua kutumia chanjo ya Johnson & Johnson.