Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma
Waratibu wa Huduma Ndogo za Fedha nchini wameipongeza Serikali kwa kuanzisha utaratibu mzuri wa kusimamia biashara ya huduma hiyo ambayo inatumiwa na wananchi wengi hususani wale wa kipato cha chini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika awamu ya pili ya mafunzo ya waratibu hao walieleza kuwa utaratibu huo utaleta mageuzi katika huduma ndogo za fedha kwa sababu kuteuliwa kwao kuratibu shughuli hizo kutasaidia wananchi wengi kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa nchi.

Afisa Biashara wa Mkoa wa Mara, Bw. Gambales Timotheo ni miongoni mwa waratibu hao ambae ameeleza kuwa mafunzo wanayopatiwa yatawawezesha kusimamia miongozo iliyotolewa na Serikali ili kukabiliana na changamoto zote zilizokuwa zinaikabili sekta ndogo ya fedha.

“Kipindi cha nyuma hizi biashara zilikuwa zikijiendesha bila kufuata utaratibu na kusababisha madhara kwa watumiaji na watoa huduma, elimu tulioipata itatuwezesha kusimamia biashara hii kwa kuwanuafaisha wadau wote muhimu ikiwemo wawekezaji, watumiaji na Serikali pia”, alibainisha.

Naye Bi. Eveline Mbwilo kutoka Wilayani Kiteto mkoani Manyara, alisema mafunzo hayo ni ya kipekee ambayo yataiwezesha Serikali kutambua wigo wa mzunguko wa fedha za wananchi na mchango wa Huduma Ndogo za Fedha katika pato la Taifa.

Awali akifungua mafunzo hayo, Kamishna wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja aliwataka waratibu hao kutumia mafunzo hayo kusimamia na kuyaweka katika mfumo rasmi mambo yote muhimu katika Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha ili yaweze kukuza ajira, kuondoa umaskini na kuboresha maisha ya wananchi hususani wale wa kipato cha chini.

Alisema Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wadau wengine  inatambua kuwa waratibu hao wanaenda kusimamia sekta nyeti katika uchumi wa nchi hiyo elimu waliyoipata ikawe chachu ya kukuza maendeleo ya Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kwa kuwaelimisha  wananchi wengine kuhusu fursa mbalimbali zilizopo kwenye biashara hiyo.

Dkt. Mwamwaja alisema mafunzo hayo yamelenga kujenga uelewa kwa waratibu wa biashara ya huduma ndogo za fedha katika ngazi ya Wizara, Mkoa na Halmashauri ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha.

“Mafunzo haya yatawawezesha waratibu kuratibu masuala yote yanayohusu sekta hii katika maeneo yao, kutengeneza na kusimamia kanzidata ya huduma ndogo za fedha, kuhamasisha biashara hiyo, kufuatilia na kutathmini maendeleo yake, kufanya usajili wa wahamasishaji na kutoa vibali kwa wahamasishaji, na kuwasilisha taarifa za huduma ndogo za fedha kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha”, abainisha.

Kuteuliwa kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo ya Fedha ni utekelezaji wa majukumu ya Waziri mwenye dhamana ya fedha kwa mujibu wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha mwaka 2018 na Kanuni zake (majukumu ya Waziri) za mwaka 2019.