Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Dodoma.
Serikali imeteua Waratibu wa kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kwa lengo la kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa Sekta Fedha nchini.

Hayo yalielezwa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru, wakati wa ufunguzi wa awamu ya kwanza ya mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha.

Alisema uteuzi wa Waratibu hao ni utekelezaji wa majuku ya Waziri wa Fedha kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 Kifungu namba 15 pamoja na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha (Majukumu ya Waziri) za mwaka 2019.

“Majukumu ya Waratibu hao yatakuwa ni kuratibu, kuhamasisha na kutathmini biashara ya huduma ndogo za fedha katika ngazi ya Wizara, Mkoa na Halmashauri pamoja na kusajili wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za fedha (Microfinance Business Promoters) pamoja na kuandaa taarifa za Sekta Ndogo ya Fedha kwa vipindi tofauti ”, alisema Bw. Ndunguru.

Alisema katika kuwawezesha Waratibu walioteuliwa kutekeleza majukumu yao kwa umakini na ufanisi, Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa mafunzo ya awamu mbili kwa Waratibu 212 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Aliwataka Waratibu hao kutumia mafunzo hayo kuimarisha na kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha katika maeneo yao ya kazi kwa maendeleo na maslahi ya wananchi hususani wenye kipato cha chini, ili waweze kuboresha maisha yao, kuondoa umaskini, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa.

Awali Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, alisema lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha.

Alisema pamoja na mambo mengine Waratibu watatengeneza na kusimamia kanzidata ya huduma ndogo za fedha, kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha na kufuatilia na kutathmini maendeleo ya biashara hizo.

Dkt. Mwamwaja alisema Waratibu hao watasajili na kufuta usajili wa wahamasishaji pamoja na kuandaa na kuwasilisha taarifa za huduma ndogo za fedha kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha.

Mafunzo hayo ni muendelezo wa jitihada za Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wadau katika kutatua changamoto zilizopo katika sekta ndogo ya fedha ili kuwezesha huduma za fedha kuwafikia wananchi wengi waishio maeneo ya vijijini na kutimiza lengo la Serikali la kuondoa umaskini na kukuza uchumi.