Na Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  amesema kuwa Serikali itashughulikia na kufuta  kodi inayotozwa katika kemikali zinazotumika kuondoa manyoya kwenye ngozi wakati wa uchakataji wa ngozi.

Akizungumza jana, mkoani Morogoro Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati akifungua kiwanda cha ngozi cha Ace Leather Tanzania Limited kilichopo Kihonda  mkoani  Morogoro, alisema kuwa  Serikali itashughulikia  na kufuta tozo iliyopo  katika  kemikali zinazotumika kuondoa manyoya ili kuifanya  ngozi iwe kwenye ubora wakati wa uchakataji ngozi.

“Kemikali zinazotumika kuondoa manyoya ili ngozi iwe kwenye ubora hii tutashughulikia kama Serikali, wizara ya Viwanda mkafanyie kazi ili hizi kemikali zinazokuja kwenye viwanda vya ngozi tu tuzifutie kodi ili waweze kuchakata ngozi zetu. kuna ngombe zaidi ya milioni 34,  mbuzi zaidi ya milioni 21 ngozi zote hizi,  hata samaki  Sangara wa Mwanza wana ngozi na zinatumika kutengenezea viatu” alisema Rais Magufuli

Kuhusu malighafi za ngozi kuuzwa nje ya nchi, Rais Maguguli alisema kuwa ukiwa na kiwanda hautauza malighafi nje, ukifanya hivyo maana yake umesafirisha ajira na fedha kwa watakaoenda kuchakata nje ya nchi.

Alisisitiza “Suala la vibali kwa wanaosafirisha ngozi ghafi nje ya nchi  hilo linaweza kufanyiwa kazi na wizara ya Mifugo,  mnawatoza asilimia 80, watozeni asilimia 100 ili waache kusafirisha ngozi ghafi nje ya nchi hiyo inaweza ikawa njia ya kuzuia watu wasipeleke ngozi ghafi nje kwa kuwa viwanda vipo na uwezo wa kuchakata ngozi upo”

Aidha, Rais Magufuli alimpongeza, Rostam Aziz,  Mwekezaji wa kiwanda cha Ace Leather Tanzania Limited kwa kuanzisha kiwanda hicho ambacho  kitazalisha ajira 1,000 na kumtaka kuzingatia maslahi nay a wafanyakazi pamoja na vifaa.

Sambamba na hilo Rais Maugufuli ameitaka benki ya CRDB ku hakikisha  kiwanda cha Canvas  kinaanza  kufanyakazi. Vilevile Rais Magufuli  Wizara ya Fedha kuhakikisha kiwanda cha Moproco kinafanyakazi.

“Nazungumza hapa mawaziri mpo, msiangaike kuleta waraka kwenye Baraza la Mawaziri  watafute mwekezaji  nije niitwe siku moja kufungua kiwanda cha Moproco kinachotengeneza mafuta ili kitengeneze ajira kwa watu wa Morogoro na watanzania.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Viwanda  kuvichukua viwanda ambavyo viko kwa wawekezaji na havijaendelezwa.

Mwekezaji wa Kiwanda cha ngozi cha Ace Leather Tanzania Limited, Rostam Azizi  alisema kuwa kiwanda hicho ni kikibwa  na chenye vifaa vya kisasa zaidi  barani Afrika ambacho cha kina uwezo wa kuchakata ngozi hadi hatua ya mwisho kwa kiwango  cha mwisho cha asilimia 65 ya ngozi zote za ngombe zinazozalishwa nchini na  ngozi za mbuzi na kondoo zinazozalishwa ncjhini kwa asilimia 100  na kitazalisha ajira 1,000.

“Mheshimiwa Rais sera zako ndizo zilizotusukuma kuwekeza takribani bilioni 50 katika kufufua kiwanda hiki, umekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kusisitiza wawekezaji hasa wa ndani wawekeze ili uchumi wetu uweze kuboreka” alisema Rostam