Na Matias Canal, Wizara ya Katib na Sheria-Dodoma
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Pinda amewahakikishia watanzania kuwa Serikali haina Sheria Kandamizi hivyo Sheria zote zinazotumika nchini zilitungwa na Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo halijawahi kutunga Sheria Kandamizi.

Amesema kuwa Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wakati na watu wake, imekuwa ikiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria mbalimbali ili kuziboresha Sheria hizo.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe Zainab Katimba aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kurekebisha baadhi ya sheria kandamizi kwa wanawake ili ziendane na wakati, Mhe Pinda amesema kuwa Kutokana na wakati uliopo na mahitaji ya sasa Serikali imeanzisha mchakato wa kuzipitia baadhi ya sheria ili ziweze kufanyiwa marekebisho kuendana na wakati.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeandaa muswada wa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa utakaowasilishwa Bungeni ili kuiboresha, kwa lengo la kulinda makundi ya wanufaika na Sheria hiyo.

Aidha, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mirathi na Sheria za Kimila. Hatua hizo zikikamilika, Muswada wa mapendekezo ya kuzirekebisha sheria hizo utawasilishwa Bungeni, ili Wabunge wapate nafasi nzuri ya kujadiliana na kuyapitisha marekebisho hayo.  

Mhe Pinda amesem akuwa Wizara ipo katika mabadiliko makubwa ya kuhakikisha kunafanyika maboresho makubwa ya Sheria zetu ikiwemo kuzitafsiri kwa Kiswahili lakini pia kuweka vipengele kwenye sheria hizo vya kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili jambo ambalo litaleta tija kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu.

Hivyo amewaomba wabunge kuunga mkono juhudi za Serikali katika eneo hilo kwa lengo la kuimarisha utawala wa Sheria na upatikanaji wa haki nchini.