Na Mwandishi Wetu- MAELEZO

Kama uko Dodoma, Iringa, Singida, Manyara, Morogoro au hata Dar maana Shabiby lipo hadi saa tisa alasiri kama hautafika Dodoma leo usinilaumu!!!!

Sasaaaa, sikiliza jana usiku wa kuamkia leo Jumamosi Februari 6, 2021, dunia ilisimama, burudani ilitambulishwa na wanaojua burudani waliburudika.

Hiyo ilikuwa show kabla ya shughuli yenyewe  leo (kwa lugha ya Shilole wanaita Serengeti Royal Pre-Party), ambapo wasanii 10 tu, kati ya zaidi ya 70 watakaotumbuiza leo, jana walitoa burudani ya kipato cha kati.

Kutoka kumbukumbu ya Awena ya Kassim Mganga, Mama Amina ya Marioo, Taabasamu ya Mr. Blue mpaka Number One ya Nandera aka Nandy, Serengeti Festival linakwenda kuwa Tamasha Number One nchini.

"Sasa kilichofanyika jana ni tone tu watu waje Jamhuri Stadium leo "walisema wasanii kadhaa waliopanda jukwaani.

Hiyo jana Shamra shamra za tamasha hilo zilitanguliwa na michezo miwili iliyochezwa katika Uwanja wa Jamhuri  jijini Dodoma kushamirisha tamasha lenyewe linakalofanyika leo.

Mechi zote mbili ziliisha kwa sare ya kutokufungana (0-0) kwa timu za mashabiki wa timu za Simba na Yanga pamoja na timu za Wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao watatumbuiza na kushamirisha tamasha la Serengeti pamoja na timu inayoundwa na Viongozi wa Serikali ya wanachuo kutoka vyuo vikuu vilivyopo mkoa wa Dodoma.

Mechi ya kwanza ilihusisha timu iliyoundwa na mashabiki wa timu za Simba na Yanga ambao ni madereva waendesha bodaboda na bajaji jijini Dodoma ambapo timu ya mashabiki wa Yanga waliibuka kidedea kwa kuwafunga mashabiki wa timu ya Simba kwa mikwaju ya penati 8-7 baada ya timu hizo kutoshana nguvu kwa kutokufungana (0-0).  

Wakati mechi ya pili ilihusisha timu za Wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao watatumbuiza na kushamirisha tamasha la Serengeti dhidi ya timu inayoundwa na Viongozi wa Serikali ya wanachuo kutoka Vyuo Vikuu vilivyopo mkoa wa Dodoma ambapo timu ya Wasanii imeibuka kidedea kwa kushinda penati 3-2 huku mlinda mlango wa timu ya wasanii Khalid Ramadhan (Tundaman) alipangua penati moja.

Hivyo basi, leo usipange kukosa kwa mtonyo wa buku tatu (3000/) utapata burudan ya kipato cha kati yenye wasanii zaidi ya 70 kuanzia saa 10: 00 jioni.