Rais wa Benki kuu ya Ulaya Christine Lagarde amepinga miito juu ya kuyafuta madeni ya nchi za ukanda wa sarafu ya Euro zinazohitaji kuimarisha uchumi wakati huu wa janga la corona. 

Watalaamu wa uchumi zaidi ya 100 barani Ulaya wametoa wito huo juu ya kufuta madeni ili kuimarisha juhudi za kurejesha ustawi wa uchumi. 

Lagarde amesema kufutwa kwa madeni ni jambo lisilowezekana kwa sababu itakuwa ni kukiuka mkataba wa Ulaya unaokataza kuzifadhili nchi kwa fedha. Ameeleza kuwa mkataba huo ni nguzo mojawapo iliyowekwa katika kuunda umoja wa sarafu ya Euro. 

Hata hivyo Benki kuu ya Ulaya imeshachukua hatua za pekee kwa ajili ya kupoza makali ya athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la corona, kwa kuzindua mpango wa kununua hatifungani thamani ya Euro trilioni 1.85 hadi sasa.