Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema kifo cha Dk Mohamed Seif Khatibu ni pigo kwa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Waziri huyo wa zamani aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini na ndani ya CCM alifariki dunia jana Jumatatu Februari 15, 2021mjini Unguja, Zanzibar.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter Kikwete ameandika;“Nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Comrade Mohamed Seif Khatibu. Nimepoteza rafiki wa karibu wa tangu ujana hadi uzee wetu. Tumefahamiana nae tangu 1982 tulipochaguliwa kwenye uongozi wa taifa wa UVCCM

“Baada ya kunganishwa kwa TANU Youth League na ASP Youth, yeye akawa Mwenyekiti wa kwanza wa Taifa na mimi nikiwa miongoni wa Wajumbe wa Kwanza wa Kamati ya Utekelezaji ya Taifa.Tangu wakati huo mpaka sasa amekuwa mtu wangu karibu katika maisha yangu ya kisiasa na hata kijamii

“Tarehe 8 November 1988 tuliteuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi kuingia kwenye Baraza la Mawaziri. Yeye alikuwa Waziri wa Nchi Ofsi ya Makamu wa Pili wa Rais na mimi nikawa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepoteza moja wa makada wake mahiri na jasiri.

“Taifa limepoteza mzalendo wa dhati na mtetezi shupavu wa Mapinduzi ya 1964. Nawatakia wana familia wake moyo wa subira na ustahamilivu. Ninamuombea mapumziko mema peponi.” -Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete