Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo ameungana na Waumini wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay Jijini Dar es Salaam kusali Misa Takatifu ya Jumapili (Dominika ya 1 ya Kwaresma) na amewashukuru Watanzania kupitia Madhehebu yao ya Dini kwa kuitikia wito wa maombi na kufunga ili Mungu aepushe ugonjwa wa Korona unaosababisha vifo vya watu duniani.

Rais Magufuli amesema Wakristo ambao wapo katika kipindi cha Kwaresma na Waislamu ambao wanakaribia kuingia katika kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, waendelee kumuomba Mungu kwani pamoja na jitihada za kibinadamu za kukabiliana na ugonjwa huo, Mungu ndiye muweza wa yote na husimama kwa kila jambo.

Amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Korona kama zinavyoelekezwa na Wataalamu wa afya na amefafanua kuwa Serikali haijazuia matumizi ya barakoa katika kujikinga kuambukizwa virusi vya Korona bali Watanzania wachukue tahadhari kwa kutumia barakoa zinazotengezwa hapa nchini zikiwemo za Bodi ya Dawa (MSD) au zinazotengezwa na Watanzania wenyewe kwa kuwa barakoa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi zina mashaka ya kuwa sio salama.

Aidha, Rais Magufuli amesisitiza kutumia njia za asili za kukabiliana na magonjwa ya kupumua ukiwemo ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kujifukiza (kupiga nyungu).

Rais Magufuli amewataka Watanzania kuondoa hofu inayopandikizwa ambayo ina madhara zaidi, na amesisitiza kuendelea kumtumaini na kumtanguliza Mwenyezi Mungu kwa kuwa njia za kujikinga kwa barakoa, kutogusana na kutokaribiana (social distancing) pamoja na kujifungia majumbani (lockdown) vimeonekana kutokuwa suluhisho la uhakika kwani Mataifa yanayofanya hivyo watu wake wanapoteza maisha kwa maelfu ikilinganishwa na hapa Tanzania.

Amempongeza Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro, Oysterbay Padre Dkt. Alister Makubi kwa mahubiri yaliyoeleza namna Yesu alivyojaribiwa na kwamba hata changamoto za sasa ikiwemo ugonjwa wa Korona ni majaribu ambayo yatapita


.