Rais Dkt. Magufuli ametangaza kuwa anakusudia kulivunja Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi moja ya manispaa za mkoa huo iwe ndiyo jiji.

Dkt. Magufuli amedokeza hilo wakati akizungumza na wananchi katika hafla ya uzinduzi wa Daraja la Juu (Interchange) la Kijazi ambalo awali lilikuwa likifahamika kwa jina la Ubungo Interchange.

Amesema Jiji la Dar es Salaam halina eneo linaloliwakilisha kwani maeneo yote ya jiji yapo chini ya manispaa, jambo ambalo linapelekea matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kuwa na viongozi ambao hawawakilishi eneo lolote.

“Kuwa na madiwani ambao wanakaa hapa juu, wanachangiwa hela, hawana miradi ya maendeleo, wanakula posho na hawakuchaguliwa na watu, hili nitalikata,” ameeleza Dkt. Magufuli.

Ameongeza kuwa, kuliko kuwatengea fedha madiwani ambao hawawakilishi watu, lakini wanaripoti kwenye manispaa zao, ni heri fedha hizo zikatumika kwenye shughuli za maendeleo ya barabara.

Amefichua kwamba tayari ameshapelekewa rasimu ya mpango huo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo na kwamba ataisaini karibuni.

“Jiji la Dar es Salaam litaendelea kuwepo lakini tutachukua eneo fulani, na ninafikiri Ilala inafaa kuwa jiji, ndiyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam,” amefafanua.

Amebainisha kuwa lengo la kufanya hayo yote ni kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya fedha za umma.