Rais Dkt. John Magufuli amezindua kiwanda cha ngozi (Ace Leather Tanzania Limited) mkoani Morogoro ambacho kitatumika kuchakata ngozi za mifugo na kuzalisha bidhaa mbalimbali za ngozi.

Akitoa taarifa za kiwanda hicho, mfanyabiashara Rostam Aziz amesema kuwa kiwanda hicho ni kikubwa zaidi barani na Afrika na kwamba kina uwezo wa kuchakata asilimia 65 ya ngozi zote za ng’ombe nchini na 100% ya ngozi za mbuzi na kondoo.

“Hiki ni kiwanda kikubwa zaidi katika bara zima la Afrika na mashine zake ni za kisasa kabisa kuliko kiwanda chochote Afrika,” amesema Rostam wakati akitoa taarifa za kiwanda hicho.

Kwa upande wake Rais Dkt. Magufuli amempongeza sana mfanyabiashara huyo kwa uwekezaji huo mkubwa ambao unatarajiwa kutoa ajira kwa watu 1000 pamoja na kupunguza usafirisha wa ngozi ghafi nje ya nchi.

Aidha, ametumia jukwaa hilo kumkosoa Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdul-Aziz Abood kwa kutoendeleza viwanda alivyomilikishwa na serikali kwa zaidi miaka 20 na hivyo kuwakosesha ajira wakazi wa mkoa huo.

Amemtaka yeye pamoja na benki ya CRDB ambayo nayo inamiliki kiwanda cha Canvas kuhakikisha vinaendelezwa na endapo wakiona hawawezi, basi wizara ya viwanda itafute muwekezaji mwingine aviendeleze.

Wakati huohuo amezindua kiwanda cha kukoboa mpunga, Murzar Wilmar Mills kilichopo Kihonda mkoani humo. Kiwanda hicho kwa siku kina uwezo wa kukoboa tani 280 za mpunga ambao unanunuliwa kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Amewapongeza wawekezaji kwa ujenzi wa viwanda na kusema kuwa hilo ni lengo la serikali yake kwani kwa kupitia viwanda wananchi wanapata ajira.