Makundi makubwa ya watu yamekusanyika nchini Myanmar leo kuendelea kulaani mapinduzi ya kijeshi ya Februari mosi licha ya ukandamizaji uliofanywa jana na vikosi vya usalama na kusababisha vifo vya waandamanaji wawili.

Mamia kwa maelfu ya watu walikusanyika kwa amani kwenye mji wa pili kwa ukubwa wa Mandalay, eneo ambalo mauaji ya waandamanaji yalitokea.

Wakati hayo yakijiri mtandao wa kijamii wa Facebook umetangaza kuufuta ukurasa unaoendeshwa na jeshi la Myanmar kwa madai ya kukiuka kanuni za maudhui kwa kuchochea vurugu na kusambaza habari za uzushi.

Jeshi la Myanmar limeshindwa hadi sasa kudhibiti wimbi la maandamano yanayopinga majenerali kuchukua madaraka na yanayotaka kuachiwa huru kwa kiongozi wa kiraia aliyepinduliwa Aung San Suu Kyi.