Polisi mjini Moscow wameanza kuwakamata watu waliokusanyika nje ya mahakama, inayotarajiwa kutoa hukumu dhidi ya mkosoaji wa Kremlin Alexai Navalny leo Jumanne. 

Mahakama mjini Moscow imeanza kusikiliza hoja za iwapo kiongozi huyo anapaswa kufungwa miaka kadhaa jela, katika mashitaka ambayo yamechochea maandamano ya nchi nzima na mazungumzo ya vikwazo vipya vya nchi za magharibi. 

Navalny mwenye umri wa miaka 44, alikamatwa Januari 17 wakati alipokuwa akirejea kutoka Ujerumani, ambako alitumia muda wa miezi mitano akitibiwa katika madai ya kupewa sumu na Kremlin. 

Mamlaka ya magereza ya Urusi inadai kuwa mwanasiasa huyo alikiuka adhabu yake iliyosimamishwa inayohusu utakatishaji fedha mwaka 2014. 

Navalny na timu yake ya mawakili wanadai kuwa wakati akipatiwa matibabu Ujerumani asingeweza kuripoti kwa mamlaka za Urusi kama ilivyotakiwa.