Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis, ametoa wito wa kuachiwa mara moja kwa viongozi wa kisiasa waliofungwa wakati wa mapinduzi nchini Myanmar. 

Hii ni mara ya pili kwa kiongozi huyo wa Kanisa kuingilia kati kuhusu Myanmar katika muda wa siku mbili, baada ya kutumia misa yake ya Jumapili kuelezea mshikamano na watu wa nchi hiyo alioizuru mwaka 2017. 

''Siku hizi fikira zangu zinakwenda hasa kwa watu wa Myanmar ambao kwao naeleza mapenzi na ukaribu wangu. 

Njia iliyochukuliwa kuelekea demokrasia katika miaka ya karibuni ilivurugwa ghafla na mapinduzi ya kijeshi ya wiki iliyopita. 

Hii imesababisha kufungwa kwa viongozi kadhaa wa kisiasa ambao natumai wataachiwa mara moja kama ishara ya dhati ya majadiliano kwa ajili ya manufaa ya taifa,'' alisema Papa Francis. 

Majenerali wa Myanmar wametoa onyo kali dhidi ya maandamano zaidi leo, huku wakitangaza sheria ya kijeshi katika miji kadhaa ya mkoa wa Mandalay. 

Shinikizo linazidi kuongezeka dhidi ya majenerali hao, kupitia maandamano ya umma kudai kuachiwa kwa viongozi wa kiraia na kurejesha demokrasia.