Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Ofisi ya Ardhi mkoa wa Morogoro imeanza kuwabana wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi kwa kuwafikisha wadaiwa sugu 50 wanaodaiwa kiasi cha shilingi 1.552,436,750 katika Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ikiwa ni mkakati wa ofisi hiyo kukusanya madeni na malimbikizo mengine ya ardhi yanayofikia trilioni 1.029.
Akizungumza ofisini kwake mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa Frank Mizikuntwe alisema kuwa, wadaiwa waliofikishwa kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ni sehemu ya wadaiwa wa kodi ya ardhi 474 aliowaeleza kuwa kufikia tarehe 8 Machi 2021 mashauri yao yatakuwa yamesikilizwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya.
Alisema, kati ya wadaiwa 50 waliofikishwa Baraza la Ardhi la wilaya ni wadaiwa 21 tu ndiyo waliojitokeza kusikiliza mashauri yao ambao hata hivyo kwa kujibu wa Frank walikubali kulipa malimbikizo yao kwa awamu kufikia mwisho wa mwezi juni 2021.
Aliongeza kwa kusema kuwa, kwa wale wadaiwa wasiofika kusikiliza mashauri yao sambamba na watakaoshindwa kukamilisha madeni katika muda waliokubaliana ofisi yake itasubiri amri ya Baraza kwa hatua zaidi ambapo maamuzi yake ni kunadiwa mali za wadaiwa kufidia deni.
Alisema, ofisi ya ardhi mkoa wa Morogoro katika kuwafuatilia wadaiwa sugu imeelekeza nguvu kubwa katika halmashauri zenye madeni makubwa ambapo alizitaja kuwa ni Manispaa ya Morogoro trilioni 1.006, Ifakara TC bilioni 11, Kilosa bilioni 6 pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mvomero shilingi bilioni 3.8
“Ofisi yangu imejipanga kuhakikisha inasambaza ilani za madai kwa wadaiwa wote wa kodi za ardhi katika mkoa wa morogoro lli tuweze kufanikisha azma ya kukusanya kiasi cha fedha kinachodaiwa kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2020/ 2021” alisema Mizikuntwe
Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro, baadhi ya mikakati inayotumika kufuatilia wadaiwa ni pamoja na kupita katika mitaa kila siku za jumatatu na ijumaa na kusambaza hati za madai na wakati huo ofisi yake ikitoa gari siku moja kwa wiki katika halmashauri kuwawezesha maafisa ardhi wa halmashauri kuwafuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi.
Ufuatiliaji wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ni utekelezaji wa Maagizo ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula aliyezitaka ofisi za ardhi za mikoa kuhakikisha wadaiwa wote sugu wa kodi za ardhi wanafikishwa kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ili walipe madeni kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2020/ 2021.