Tume ya umma nchini Urusi inayoangalia haki za binaadamu za wafungwa nchini Urusi imesema mkoasoaji mkubwa wa serikali ya Urusi Alexi Navalny, amepelekwa katika jimbo la Vladimir kilomita 200 kutoka Mashariki mwa Moscow kutumikia kifungo chake cha miaka miwili na nusu jela. 

Mwanachama wa tume hiyo Alexei Melnikov amesema wana uhakika kuwa Navalny amehamishiwa eneo la Vladmir. 

Mkosoaji huyo mkubwa wa rais Vladimir Putin alihukumiwa kifungo hicho kwa makosa ya kukiuka masharti ya msamaha wa kuachiwa mapema kutoka jela wakati alipokuwa Ujerumani akipata matibabu baada ya kupewa sumu ya Novichock inayoathiri mishipa ya fahamu. 

Kwa siku kadhaa washirika wake hawakujua aliko Navalny huku mkuu wa magereza akisema ametolewa mjini Moscow na kupelekwa katika eneo la nje la wafungwa bila kutoa maelezo zaidi. 

Navalny anadai alipewa sumu kwa maagizo kutoka kwa rais Putin, madai ambayo serikali ya Urusi inaendelea kukanusha.