Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Abdallah Ulega amewataka wazalishaji wa bidhaa za ndani kuandika kwa Kiswahili maelekezo ya matumizi ya bidhaa wanazozalisha ili Watanzania waweze kuzisoma na kuzielewa.
 
Akizungumza katika ziara yake aliyofanya leo Februari 15, 2021 katika ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Mhe. Ulega amewataka wazalishaji mbalimbali wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania kutumia Kiswahili katika maelezo yao ili bidhaa zipate kueleweka kwa watumiaji.

“Wazalishaji wote wa ndani na wa nje wanaoingiza bidhaa zao nchini waangalie namna bora ya matumizi ya lugha ya Kiswahili kwenye bidhaa zao ambazo nyingi zinaandikwa kwa lugha ya kigeni ili kuwawezesha Watanzania kuelewa maelekezo husika yaliyoko kwenye bidhaa hizo” alisema Naibu Waziri Ulega.
 
Ulega ameitaka BAKITA kusimamia ipasavyo zoezi hilo ili kuhakikisha Watanzania wanatumia bidhaa wanazozijua tofauti na sasa ambapo bidhaa nyingi zimeandikwa kwa lugha tofauti na Kiswahili.
 
 Aidha, Naibu Waziri Ulega ametoa mwezi mmoja kwa BAKITA kusimamia na kudhibiti  mfumo wa mapato yatokanayo na ithibati ya lugha ya Kiswahili ili kuongeza mapato ambayo yamekuwa yakipotea kila siku kutokana na kuwepo kwa watafsiri wengi wa lugha ya Kiswahili wasiokuwa na ithibati.
 
Kufuatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Bungeni Februari 11, 2021, kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki la kuitaka Wizara hiyo kuanzisha madarasa ya lugha ya Kiswahili kwa wageni wanaoingia nchini, Naibu Waziri Ulega ameitaka BAKITA kushirikiana na Wizara hiyo kuangalia namna ya kuanzisha madarasa hayo mapema iwezekanavyo.

“Hivi karibuni Waziri Mkuu alitoa maagizo kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuanzisha madarasa ya lugha ya Kiswahili kwa wageni, nawataka BAKITA mshirikiane nao kuhakikisha madarasa hayo yanaanzishwa”, alisisitiza Naibu Waziri Ulega.
 
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolata Mushi amesema Malengo na mikakati ya kufanikisha majukumu ya baraza hilo yamebainishwa katika mpango mkakati wa Mwaka 2020-2021 hadi 2024-2025 kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya ndani na  nje ya nchi ambayo yanalenga kufikia Dira ya Taifa ya mwaka 2025.
 
“Malengo ya BAKITA, ni kuona Tanzania ikiwa ni nchi yenye watu walioelimika vya kutosha ifikapo 2025 huku Kiswahili kikiwa ni mojawapo ya zana za kimkakati za kufikia lengo hilo”, alisema Bi.Mushi.
 
Mwisho.