Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezitaka idara za ardhi katika halmashauri za mkoa wa Shinyanga kuwatambua wamiliki wote wa ardhi ambao ramani za upimaji wa viwanja vyao umeidhinishwa na kuanza kuwatoza kodi ya pango la ardhi kwa mujibu wa sheria.
Dkt Mabula alitoa agizo hilo leo tarehe 01 Januari 2021 mkoani Shinyanga wakati wa ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi, kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi pamoja na kukutana na makampuni ya urasimishani.
” kila halmashauri katika mkoa huu wa Shinyanga ichukue hatua kwa kuwatambua wamiliki wote wa viwanja ambao approved survey imefanyika na kuanza kuwatoza kodi ya pango la ardhi” alisema Dkt Mabula.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula kwa sasa hakuna suala la kubembeleza wakati wa kufuatilia wadaiwa wa kodi ya ardhi na kusisitiza kuwa shilingi bilioni 1.3 sawa na asilimia 22 zilizokusanywa kufikia Desemba 2020 kama kodi ya ardhi katika mkoa wa Shinyanga ni ndogo na aibu kwa mkoa.
Aidha, aliwataka Maafisa Ardhi katika halmashauri za mkoa wa Shinyanga kuwafutia viwanja wamiliki wa adhi waliokaidi kulipa kodi ya pango la ardhi hata pale walipopelekewa ilani za madai baada ya miezi sita.
kwa mujibu wa kifungu Na 48(1) (g) cha sheria ya ardhi, Afisa Ardhi anayo mamlaka ya kufuta umiliki wa ardhi kwa mmiliki aliyekaidi kulipa kodi ya pango la ardhi katika kipindi cha miezi sita baada ya kutumiwa ilani ya madai.
“Hatua zisipochukuliwa katika suala lla kudai kodi ya ardhi kwa wadaiwa sugu hatutaitendea haki Tanzania katika mapato ambayo yanamsaidia mhe Raisi John Pombe Magufuli kutekeleza miradi ya maendeleo”. Alisema Naibu Waziri Mabula.
Aidha, Naibu Waziri Mabula katika ziara yake alitoa hati kumi na moja kati ya kumi na tisa kwa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga na kuwataka waliokabidhiwa hati kuhakikisha wanalipa madeni yao katika kipindi cha siku kumi nne na wasipofanya hivyo wafikishwe kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwa hatua zaidi.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Dkt Mabula faida ya hati ni pamoja na kuwa na usalama wa miliki, kuepuka migogoro ya ardhi inayoweza kusababishwa na mipaka pamoja na kuitumia hati katika shughuli za maendeleo kwa kuchukulia mkopo benki.
Naye Mwananchi wa Manispaa ya Shinyanga Bw. Kadama John alifika mbele ya kikao cha Naibu Waziri Mabula na kudai kuwa wataalam wa ardhi Mkoani Shinyanga waligawa kiwanja chake kwa wananchi watatu na kuwapa umiliki hivyo yeye haoni sababu yakuletewa madai jambo ambalo Naibu Waziri aliamua kuwa wote wamilikishwe na kugawana deni hilo kama shart la kumilikishwa ardhi.