Jeshi la Myanmar limemfuta kazi balozi wake katika Umoja wa Mataifa kwa madai ya kutoa shutuma za kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa kiraia Aung San Suu Kyi, wakati polisi wakiongeza ukandamizaji dhidi ya waandamanaji. 

Balozi Kyaw Moe Tun anadaiwa kuwa amevunja maelekezo ya serikali baada ya kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kali na za haraka katika kurejesha demokrasia nchini Myanmar. 

Kuondolewa kwake kunafuatia siku moja ya ukandamizaji na kukamatwa kwa waandamanaji kulikofanywa na vikosi vya usalama vya Myanmar, wakati nchi hiyo ikiingia wiki yake ya nne ya maandamano ya kila siku dhidi ya utawala wa kijeshi. 

Ghasia zilizuka jana kwenye mji wa kibiashara Yangon, wakati polisi walipozuia mapema maandamano ya amani na kufyatua risasi za mipira kutawanya raia. Zaidi ya watu 770 wamekamatwa, kushitakiwa na kuhukumiwa tangu nchi hiyo itumbukie katika mgogoro.