Na Mwandishi Wetu- Unguja
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) una mchango mkubwa katika kujenga uchumi na kuondoa migogoro ya ardhi baada ya urasimishaji. 


Ameyasema hayo  Februari 11, 2021 Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA na Menejimenti  ya Mpango huo.


"Nimejulishwa kuwa Mpango huu tangu uanze hapa Zanzibar, tayari shilingi milioni 441 zimetolewa kuwezesha urasimishaji, naahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa kipaumbele kwa kutenga bajeti ili kuendekeza kazi hii ya urasimishaji ",alisisitiza Rais Dkt. Mwinyi 


Akifafanua amesema kuwa mpango wa urasimishaji utasaidia wananchi  wengi zaidi kupata mitaji ya kukuza biashara na shughuli za uzalishaji. 


Aidha, Mhe. Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Mpango huo Bi. Immaculata Senje ikiwemo kuendelea kutenga bajeti ya urasimishaji. 


"Mapendekezo yaliyotolewa na Mpango huu ndizo ahadi zangu za uchaguzi kwa wananchi ikiwemo kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kufanya kazi zao kwa tija ",alisisitiza Mhe.Rais   Dkt. Mwinyi 


Aliongeza kuwa kujengwa kwa vituo  jumuishi vya biashara vipatavyo 10 visiwani Zanzibar kutasadia kuwawezesha wananchi wengi kurasimisha biashara zao na kuondokana na adha ya urasimu , hii ikiwa ni moja ya ahadi zake wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.


Akizungumzia ahadi zake kwa wananchi Mhe.Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na; kuwezesha wananchi kupata mitaji ambapo mpango huo unatoa majibu ya changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta ya ardhi na biashara kwa kuwaunganisha na Taasisi za fedha kupitia hati zao za kumiliki ardhi. 


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA Bi. Immaculata Senje amempongeza Mhe. Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa kuchaguliwa na wananchi kwa kura nyingi. 


Aliongeza kuwa MKURABITA imepanga kusajili wajasiriamali 1500, kupima viwanja 5700 katika wilaya za Pemba na Unguja, kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa urasimishaji ardhi na Biashara .


Pia, mpango huo utaendelea kuwaunganisha wananchi na taasisi za fedha ili waweze kukuza mitaji kwa kutumia hati miliki zao za kumiliki ardhi kujikwamua kiuchumi.


Naye Mratibu wa Mpango huo CPA Dkt. Seraphia Mgembe amesema kuwa MKURABITA itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha kuwa azma ya kujenga uchumi wa buluu inatekelezwa kwa vitendo ili wananchi wafurahie matunda ya urasimishaji. 


Aliahidi kuendelea kutoa msukumo katika kuwaelimisha wananchi ili watumie rasilimali ardhi kupata mitaji kupitia hati zao baada ya urasimishaji. 


Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA wanahitimisha ziara yao Visiwani Zanzibar Februari 12, 2021, Aidha katika ziara hiyo walishiriki katika ufunguzi wa kituo jumuishi cha Biashara Darajani Zanzibar, kutoa hati miliki za kumiliki ardhi 50 kwa wakazi wa Shehia ya Welezo, kuwatembelea wanufaika wa Mpango huo na kujionea shughuli zao na manufaa waliyopata baada ya urasimishaji. 


Ziara ya wajumbe wa Kamati hiyo ilianza Februari 7,2021 na imehitimishwa kwa wajumbe hao kupata fursa ya kukutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi