Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo Cha Uhasibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), Sospeter Omollo, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashitaka 48 ikiwemo kughushi, ubadhirifu na utakatishaji fedha zaidi ya Sh milioni 400.

Omollo alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Yusto Luboroga, huku upande wa mashitaka ukiwakilishwa na Mwendesha Mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hassan Dunia, akisaidiana na Lupyana Mwakatobe.

Mwendesha Mashitaka Dunia alidai katika shitaka la kwanza hadi la 46, mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa ya kughushi. Ilidaiwa kuwa kati ya Septemba 22, 2015 na Juni 5, 2017 katika benki ya BOA Tawi la Ilala kwa nia ovu, alighushi hundi 46 zenye thani ya Sh 410,170,000. Alidai kuwa katika shitaka la 47, mshitakiwa anakabiliwa na kosa la ufujaji na ubadhirifu.

Ilidaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Septemba 22, 2015 na Juni 5, 2017 katika benki ya BOA Tawi la Ilala akiwa ni mhasibu alipokuwa ameaminiwa kama mtumishi, alifanya ubadhirifu wa Sh 410,170,000.

Katika shitaka la mwisho, mshtakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kutakatisha Sh 410,170,000, kosa analodaiwa kulitenda katika tarehe tofauti kati ya Septemba 22, 2015 na Juni 5, 2017 katika Benki ya BOA Tawi la Ilala.

Alitakatisha fedha hizo huku akijua ni mazao ya makosa tangulizi ya ufujaji na ubadhirifu. Upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kesi hiyo itarejea mahakamani Februari 16 mwaka huu kwa ajili kusomewa maelezo ya awali.

Mshitakiwa alipelekwa mahabusu kwa sababu shitaka la utakatishaji halina dhamana.