Mawaziri wa mambo ya nje wa Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Uingereza na Marekani kwa pamoja wamelaani vurugu zinazofanywa na jeshi dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani nchini Myanmar. 

Katika taarifa ya pamoja iliyomuhusisha pia mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrel, iliyochapishwa leo mawaziri hao wametowa salamu za rambirambi kutokana na vifo vilivyotokea nchini humo pamoja na kulitolea mwito jeshi na polisi kujizuia kutumia nguvu kupita kiasi pamoja na kuheshimu haki za binadamu na sheria ya kimataifa wakati wa maandamano hayo. 

Taarifa hiyo imesema matumizi ya risasi za moto dhidi ya watu wasiokuwa na silaha ni suala lisilokubalika na yeyote atakayeshughulikia maandamano ya amani kwa kutumia nguvu anapaswa kubebeshwa dhamana. Maelfu ya raia wa Myanmar wanaendesha mgomo na maandamano ya kupinga vitendo vya jeshi.