Rais wa Marekani Joe Biden ametishia kuirejeshea Myanmar vikwazo baada ya jeshi kupindua serikali.

Jeshi la Myanmar lilimkamata Aung San Suu Kyi na viongozi wengine wa kisiasa wakiwashutumu kwa udanganyifu katika uchaguzi wa hivi karibuni ambao Suu Kyi alipata ushindi mkubwa.

Katika taarifa, Biden amesema "nguvu isiwahi kutumika kubadilisha maamuzi ya watu au kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika kwa njia ya halali".

Umoja wa Mataifa na Uingereza pia zimeshutumu mapinduzi hayo.

Marekani ilikuwa imeiondolea nchi hiyo vikwazo zaidi ya muongo mmoja uliopita wakati ambapo Myanmar ilionesha kufuata demokrasia.
 

Biden amesema hatua hiyo itapitiwa tena kwa haraka na kuongeza: "Marekani itaunga mkono demokrasia kila itakapokuwa hatarini."