Na. Peter Haule na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma
Serikali hufanya maboresho ya viwango vya kodi kila mwaka ili kuongeza wigo wa kukusanya kodi na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka nje.

Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis (Mb) alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti maalum, Mhe. Stella Fiyao, aliyeuliza ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuondoa kodi kandamizi kwa wafanyabiashara na kuweka kodi Rafiki ili kumsaidia mfanyabiashara.

Mheshimiwa, Mwanaidi Ali Khamis, alisema kuwa kupitia Sheria ya Fedha ya               mwaka 2019/20, Serikali ilifuta tozo na ada 54 zilizotozwa na Wakala, Taasisi na Mamlaka mbalimbali za Serikali ambazo hazikuwa Rafiki.

“Napenda kuchukua fursa hii kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano haitozi kodi kandamizi na itaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara ikiwa ni pamoja na kuongeza vivutio na fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wazawa na wawekezaji kutoka nje”, alieleza Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kupitia na kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi kwa kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Ufanyaji wa Biashara nchini (Blueprint for Regulatory Reforms to Improve Business Environment) wenye lengo la kurahisisha mazingira ya kufanya biashara.

Kwa upande mwingine, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imelichukua ombi la wananchi wa jimbo la Tunduru Kusini la kufungua ofisi za Mamlaka hiyo ili kupereka huduma karibu na kurahisisha ulipaji na ukusanyaji kodi.

Alibainisha kuwa suala la kufungua ofisi za TRA eneo hilo, litafanyiwa kazi kwa kutuma timu ya wataalam ili kufanya tathimini ya kina na endapo kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa kitakuwa kikubwa ikilinganishwa na gharama za ukusanyaji wa mapato, ujenzi wa ofisi utaanza haraka.

‘’TRA inaoutaratibu wa kufanya tathmini ya eneo la kujenga ofisi zake kwa kuzingatia uwiano wa gharama za ukusanyaji wa mapato na kiwango cha kodi kinachotarajiwa kukusanywa kutokana na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo’’, alieleza Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis.

Amewapongeza wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini kwa kutambua umuhimu wa kulipa kodi hivyo dhamira ya Serikali ni kutumia fursa ya ombi la kujengwa ofisi za TRA ili kurahisisha ulipaji na ukusanyaji wa kodi.

Mwisho.