Samirah Yusuph.
Bariadi. Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Simiyu imewanasa katika mtego maafisa wawili wanaotoa mikopo kwa riba kubwa bila kuwa na leseni wakitoa rushwa ya tsh 300,000 kwa afisa wa TAKUKURU wilayani Busega ili asiwachunguze.

Akizungumza na waandishi wa habari leo februari 9, 2021 ofisini kwake naibu mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Simiyu Alex Mpemba, amesema kuwa taasisi hiyo iliwakamata Ezra Simon na Yusuph Oppy wakazi wa Busega baada kumhonga fedha Msafiri Mfundo ambaye ni mfanyakazi wa takukuru.

"Mtego wa kuwanasa wakitoa rushwa uliandaliwa ili kukamilisha lengo hilo ndipo watuhumiwa walikamatwa wakitoa fedha hizo".

Baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hao walifikishwa katika mahakama ya mkoa wa Simiyu februari 4,2021, na kufunguliwa kesi ya rushwa namba CCC. 1/2021 ambapo mwendesha mashtaka wa taasisi hiyo  Carson Nkya aliiambia mahakama kuwa;

"Mtuhumiwa wa kwanza alishitakiwa kwa kosa la kushawishi rushwa na mshitakiwa wa pili alishitakiwa kwa kesi ya kutoa rushwa ya tsh 300,000".

Uchunguzi huo uliopelekea watoe rushwa hiyo ulikuja baada ya mwalimu mmoja kutoa taarifa ya kupewa mkopo na watuhumiwa hao wa milioni tano na kutakiwa kurejesha milioni 10 ndani ya muda mchache.

Ambapo baada ya mwalimu kugoma kurejesha kiasi hicho cha fedha, alirejesha kiasi cha milioni  tano alizokopa awali kisha akatoa taarifa hiyo kwa Takukuru.

Baada ya kusomewa mashitaka dhidi yao washitakiwa wote wawili walikiri mashitaka dhidi yao ambapo mahakama ili watia hatiani na kuwahukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya tsh laki tano kila mmoja.

Washitakiwa wote walilipa faini ya shilingi milioni moja pamoja aidha mahakama iliamuru fedha zilizo husika na rushwa kutaifishwa na kuingizwa kwenye mapato ya serikali.

Mwisho.