Licha ya kupungua kwa maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani, Kansela Angela Merkel hayuko tayari kulegeza masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi hivyo. 

Katika mahojiano na kituo cha utangazaji cha umma ARD, Merkel amesema kwa sasa kunaripotiwa maambukizi ya watu 100 katika kila wakazi 100,000 ndani ya siku saba. 

Ila amesema hali hiyo haimaanishi kwamba mamlaka za afya zimefanikiwa kuvidhibiti virusi vya corona. Ameongeza kwamba masharti hayatolegezwa hadi pale wakazi wote wa Ujerumani watakapochanjwa. 

Aidha Merkel ameisifu chanjo ya Urusi ya Sputnik V na kusema aina zote za chanjo zinakaribishwa katika Umoja wa Ulaya. Kansela huyo amesema ameshazungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin juu ya chanjo hiyo.