Wajumbe wa pande hasimu kisiasa nchini Libya, wamefanikiwa kumchagua waziri mkuu na wajumbe watatu wa baraza la urais, ambao wataiongoza serikali ya mpito ya kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka huu. 

Mkutano wa wajumbe hao 74 umemchagua mfanyabiashara Abdul-Hamid Mohammed Dbeibeh kuwa waziri mkuu wa mpito, na balozi wa zamani wa Libya nchini Ugiriki Mohammed Menfi kuongoza baraza la urais. 

Kuchaguliwa kwa serikali ya pamoja ya mpito kuna lengo la kumaliza mgawanyiko nchini Libya, ambapo kwa miaka mitano iliyopita nchi hiyo ilikuwa na serikali mbili; moja yenye makao mjini Tripoli ikiongoza upande wa magharibi, huku nyingine iliyoungwa mkono na makundi kadhaa yenye silaha ikiidhibiti sehemu ya mashariki ya nchi hiyo. 

Mkutano uliofanikisha uchaguzi huo umefanyika karibu na Geneva, ukisimamiwa na Umoja wa Mataifa.