Kuwa Na Tatizo Katika Mfumo Wa Hewa Sio Kuumwa Corona – Katibu Mkuu Wizara Ya Afya
Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- Mwanza.
KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewatoa hofu wananchi kwamba, kuwa na tatizo katika mfumo wa kupumua sio kuumwa ugonjwa wa Corona.
Prof. Mchembe ametoa elimu hiyo leo wakati akiongea na Waandishi wa habari, baada ya ziara yake katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa Bugando na hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya nchini.
“Watu wasiogope kwenda hospitalini, Sio kila wagonjwa ambao wanahitaji huduma ya mfumo wa hewa wanahitaji kupewa utambuzi (diagnosis) kuwa na ugonjwa wa Corona, kuna wenye kisukari, kuna wenye matatizo ya moyo na wenye presha na wakina mama wajawazito ” amesema Prof. Mchembe.
Aliendelea kusema kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure ina jumla ya vitanda 315, huku wagonjwa watano ambao wamelazwa wakisumbuliwa na magonjwa ya kisukari na moyo, huku akisisitiza kuwa wagonjwa wote wamegunduliwa kuwa na hali hiyo baada ya kufika hospitali.
“Sekou-Toure ina vitanda 315, lakini kuna wagonjwa watano ambao wamelazwa wakiwa na magonjwa ya sukari, magonjwa ya moyo, na wote hawa wamegunduliwa na kisukari wakiwa hospitalini jambo ambalo ni hatari katika Afya ya binadamu.” Amesema Prof. Mchembe.
Aidha, Prof. Mchembe amewataka wananchi kujenga tabia ya kujitokeza kupima afya zao mapema ili kutambua hali zao na kuweza kupata matibabu bila ya kuchelewa kabla ya kupata matokeo ya hali ya kushindwa kupumua.
“Ningeshauri Jamii kujitoa mapema kupima Afya zetu hata kabla ya kuwa na matokeo kama haya, kwasababu kushindwa kupumua hakuendani na sababu moja tu ya kwamba umepata maambukizi ya mfumo wa hewa, inawezekana isiwe mfumo wa hewa na ikawa moyo ndio una tatizo, au sukari imepanda, na vyote vinapelekea tatizo la kupumua ” amesema.
Pia, amewataka Watoa huduma kuwahudumia wananchi wa aina zote, huku akiamini katika hali ya utoaji huduma kwenye Hospitali hiyo hakuna mtoa huduma anaehofia mgonjwa mwenye tatizo la mfumo wa kupumua basi ana ugonjwa wa Corona.
Nae, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa Bugando Dkt. Fabian Massaga amesema kuwa, Hospitali ya Bugando inapokea wagonjwa wa aina mbali mbali wakiwemo wagonjwa wenye matatizo ya kupumua kama vile magonjwa ya pumu, magonjwa ya kisukari, magonjwa ya presha na mshtuko.
Alisema kuwa, sio kweli kuwa, Hospitali ya Bugando imejaa wagonjwa wa matatizo ya kupumua, na sio kweli wodi zimejaa wagonjwa wenye matatizo ya kupumua, ukweli ni kwamba tunawapokea wagonjwa wa aina mbali ambayo yanapelekea kuwa na matatizo katika mfumo wa hewa, mfano wenye magonjwa ya pumu na kisukari, alisisitiza hilo.
Hata hivyo, amesema kuwa, Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Ziwa Bugando imejipanga vizuri kuwahudumia wagonjwa wenye kisukari, presha, pumu ambayo yanapelekea kuwa na matatizo ya kupumua, huku akisisitiza kuwa Hospitali ina mitambo ya mikubwa miwili ya kuzalisha hewa ya oksijeni kwaajili ya kuwasaidia wagonjwa hao, jumla ya mitungi 50 mpaka 60 huzalishwa kwa siku.
Mbali na hayo, amewaondoa hofu wananchi wote kuwa, Hospitali ya Bugando hakuna tatizo lolote la Corona, hivyo kuwataka wasiogope kwenda kupata huduma za matibabu katika Hospitali hiyo na hakuna tishio lolote la ugonjwa huo.