Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema kuwa mapema leo asubuhi alifika katika hospitali ya Taifa Muhimbili kumjulia hali Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif na alikuta akiwa anaonesha matumaini ya kupata nafuu.

Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 17, 2021, masaa kadhaa tu mara baada ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi, kutangaza kifo cha kiongozi huyo wa serikali na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo kilichotokea katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

"Kwa mujibu wa taarifa ya madaktari na leo asubuhi nilikuwa hospitalini na nilionana na jopo la madaktari waliokuwa wanamhudumia Maalim Seif na kwa hakika alikuwa anaonesha matumaini ya kupata nafuu lakini ilipofika majira ya saa 5:29 asubuhi akawa amerudi kwa muumba wake", amezungumza Zitto Kabwe.

Aidha Zitto ameongeza kuwa, "Taarifa za mipango ya mazishi tutazitoa kwa umma baada ya mashauriano na masuala yake ya mazishi yanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na sisi kama chama tutatoa ushirikiano wote kwa serikali ili kuhakikisha kwamba tunamstiri mzee wetu kwa heshima anayostahili".