Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya jana  mchana tarehe 22 Februari, 2021 amekabidhi vitendea kazi kwa Watumishi wa Afya ya Mimea Kanda ya Kati vyenye thamani ya shilingi milioni 3,688,800.

Makabidhiano ya vitendea kazi hivyo yamefanyika katika ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma ambapo awali Katibu Mkuu amesema ametoa vitendea kazi hivyo mara baada ya kuwatembelea mwaka jana na kumueleza kuwa wamekuwa wakikabiliwa na ufinyu wa bajeti ya ajili ya kununua vitendea kazi hivyo.

Mratibu wa Afya ya Mimea Kanda ya Kati Bi. Happiness Lopa amemshukuru Katibu Mkuu wa kutimiza ahadi yake na kuahidi kuwa vitendea kazi hivyo vitatumika sawasawa na kusudio lake.

“Kwa niaba ya Watumishi wenzangu wa Kituo cha Afya ya Mimea Kanda ya Kati namshukuru Katibu Mkuu wa kununua vitendea kazi hivi; Ambavyo tutavitumia kwa ajili ya kutekeleza majukumu yetu ya kazi za kila. Vifaa hivi ni muhimu katika kutimiza jukumu moja kati ya majukumu yetu ya kudhibiti visumbufu vya mazao na mimea kama panzi aina ya nzige, ndege na panya.”

Vitendea kazi vilivyokabidhiwa na Katibu Mkuu kwa Watumishi hao ni pamoja na viatu vigumu (Gum boots) 10, makoti maalum (Overall) 10, vifaa vya kukinga vidole (Gloves) 20, barakoa maalum (Flits mask) 9, miwani maalum 10, makoti maalum (Reflector jacket) 20 na makoti ya mvua (Rain coat) 10.