Utawala wa kijeshi nchini Myanmar umeahidi utaitisha uchaguzi na kukabidhi madaraka. 

Hata hivyo, utawala huo umekanusha kwamba kitendo cha kuondolewa madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi kilikuwa ni mapinduzi au kwamba viongozi wake walikamatwa na wanawashutumu waandamanaji kwa kuchochea ghasia na vitisho. 

Msemaji wa baraza linalotawala, Brigedia Jenerali Zaw Min Tun amesema leo kuwa lengo lao ni kuitisha uchaguzi na kukabidhi madaraka kwa chama kitakachoshinda. 

Kauli hiyo ameitoa kwenye mkutano wa kwanza na waandishi habari tangu jeshi lilipoiondoa madarakani serikali ya Aung San Suu Kyi. Jeshi halijatangaza tarehe ya kufanyika uchaguzi mpya, lakini limetangaza hali ya hatari kwa mwaka mmoja. 

Aidha, Suu Kyi amefunguliwa mashtaka mapya ikiwemo kukiuka sheria ya usimamizi wa majanga ya Myanmar kuhusu hatua za kukabiliana na virusi vya corona. Wakati huo huo, China imekanusha uvumi kwamba inahusika kwenye mapinduzi ya kijeshi ya Myanmar.