Serikali imeutaka uongozi wa kiwanda cha sukari Kilombero kuhakikisha inaharakisha mchakato wa uwekezaji ili kuongeza uwezo wake wa kuchakata miwa yote inayozalishwa na wakulima wadogo ili nchi ijitosheleze kwa sukari.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa jana (15.02.2021) na Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda wakati alipoongea na Menejimenti ya Kampuni ya sukari ya Kilombero pamoja na wakulima wa miwa wa wilaya ya Kilombero.

Prof. Mkenda alisikitishwa na taarifa ya Bodi ya Sukari kuonesha kuwa wastani wa tani 350,000 za miwa ya wakulima wadogo sawa na tani 35,000 za sukari endapo zingechakatwa hukosa kununuliwa na wamiliki wa viwanda vya kuchakata miwa vya Kilombero huku nchi ikiendelea kuwa na upungufu wa sukari.

“Hatuwezi kuwa mateka katika suala la uzalishaji sukari kwa kumtegemea mzalishaji mmoja. Tatizo wakulima wana miwa hainunuliwi na mwekezaji halafu nchi inaendelea kutoa vibali kwa mwekezaji kuagiza sukari nje ya nchi wakati anatakiwa kuongeza uwezo wa viwanda vyake kuchakata miwa ya wakulima” alisema Waziri Mkenda.

Akizungumza na wakulima wa miwa wa wilaya ya Kilombero kwenye ukumbi wa chuo cha Taifa cha Sukari(NSI) Waziri Mkenda alisikiliza kero za wakulima waliolalamikia kitendo cha mwekezaji kampuni ya sukari Kilombero kushindwa kununua miwa yote takribani tani 800,000 inayozalishwa na wakulima ili kuchakata sukari .

Waziri huyo wa Kilimo alisema takwimu za uzalishaji miwa zinaonesha wastani wa tani 350,000 hazijanunuliwa na mwekezaji Kilombero Sugar Co. Ltd ambapo zingetosha kuzalisha sukari tani 35,000 kwa maana hiyo nchi ingeagiza nje sukari tani 5,000 pekee kati ya 40,000 za upungufu wa sasa.

Kufuatia hali hiyo Prof. Mkenda aliagiza uongozi wa kiwanda cha sukari Kilombero kuharikisha mchakato wake wa kuongeza uwezo wa kiwanda kuchakata miwa kutoka tani 629,000 mwaka 2018/2019 hadi kufikia tani 800,000 msimu huu ili miwa yote ya wakulima wadogo inayozalishwa sasa na kukosa soko itumike kuzalisha sukari.

Alibainisha mpango wa wizara yake kutaka suala la upungufu wa sukari kuisha ambapo amepongeza hatua zilizochukuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015 kudhibiti uagizaji sukari toka nje ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani

“Kabla Rais Magufuli hajaingia madarakani nchi ilikuwa ikiagiza sukari tani 125,000 toka nje lakini kutokana na hatua za udhibiti serikali imefanikiwa kupunguza uagizaji wa sukari hadi wastani wa tani 40,000 mwaka 2020 ili kutoa fursa kwa viwanda vya ndani kuzalisha “ alisema Prof. Mkenda.

Ili kuhakikisha viwanda vyote vya sukari vinatekeleza masharti yaliyomo ndani ya mikataba yao ya kubinafsishwa, Waziri Mkenda amemwagiza Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Gerald Kusaya) kuwasilisha kwake mikataba yote ya viwanda vya sukari ili ajiridhishe na utekelezaji wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero Balozi Mstaafu Ami Mpungwe alisema kiwanda hicho ni kielelezo kizuri cha faida ya ubinafishaji kutokana na kuongeza uwezo wa kuzalisha sukari kutoka tani 28,000 mwaka 1998 hadi tani 128,000 za sukari mwaka 2020 kwa viwanda vyote viwili ( Kilombero I na Kilombero II)

Balozi Mpungwe aliongeza kusema kampuni ya sukari ya Kilombero inaendeshwa kwa ubia kati ya Kilombero Holdings Ltd (Mauritius) yenye hisa asilimia 75 na serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 25 na kuwa inategemea miwa ya wakulima wadogo kwa asilimia 50 kuzalisha sukari.

“Kama kuna mtu ana fikra kuwa wakulima wadogo tunawadharau siyo kweli, tunawategemea sana ili viwanda vyetu viendelee na sasa tunalenga kufikia kununua miwa ya wakulima asilimia 60 baada ya upanuzi wa kiwanda mwaka 2023” alisisitiza Balozi Mpungwe.

Mwenyekiti huyo wa Bodi alisema tayari wameanza kushawishi wabia wake kujenga kiwanda kipya kikubwa kitakacho wezesha kuongeza uchakati wa miwa yote ya wakulima ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 584 zinahitaji na kuwa kiwanda kinatarajiwa kukamilika mwaka 2023 kitakacho kuwa na uwezo wa kuchakata tani 420 za miwa kwa saa tofauti na sasa ambapo kinachakata tani 220 kwa saa.

Takwimu za kiwanda hicho zimeonesha hadi tarehe 15 mwezi wamechakata miwa toka kwa wakulima tani 612,000 na kuwa wanatarajia ifikapo mwezi Machi watakapofunga msimu wafikishe tani 645,000 za miwa ili kuondoa changamoto za wakulima.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mikumi Lazaro Londo akiongea kwenye mkutano wa wakulima alisema wakulima wanataka miwa yao yote inayozalishwa na sasa kukosha soko takribani tani 300,000 inunuliwe yote na viwanda vya sukari ili upungufu wa sukari uishe.

Londo aliomba serikali kutoendelea kutoa vibali kwa wawekezaji wa viwanda vya miwa ikiwemo Kilombero kuagiza sukari nje kwa kuwa inapelekea wasinunue miwa ya wakulima.

“Kitendo cha kuwapa vibali wawekezaji hawa kuagiza nakisi ya sukari nje inasababisha miwa ya wakulima kukosa soko kwani kitendo cha kuagiza sukari nje makampuni yanapata faida kubwa huku wakulima wakiendelea kuwa masikini” alisisitiza Mbunge Londo.

Mmoja wa wakulima wa miwa Helina Kopa wa Kilombero akiongea kwenye mkutano huo alilalamikia kitendo cha kampuni kushindwa kununua miwa ya wakulima kwa kigezo kuwa imekaa muda mrefu baada ya kuvunwa huku akitaka serikali kuchunguza mwenendo wa uuzaji miwa unaofanywa na kampuni .

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda yupo kwenye ziara ya kikazi kukagua utendaji kazi wa viwanda vya miwa vya Kilombero, Mtibwa na Mkulazi vilivyopo mkoani Morogoro.

Mwisho
Imeandaliwa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Kilimo

MOROGORO