Na Munir Shemweta, WANMM BUKOBA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makakzi Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kununua vifaa vya upimaji ardhi ili kuongeza kasi ya upimaji katika maeneo yao.

Aliipongeza halmashauri ya Bukoba kwa uamuzi wake wa kutumia mapato ya ndani kununua vifaa vya upimaaji vyenye thamani ya shilingi milioni 34.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa vya upimaji akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji kodi ya ardhi katika mkoa wa Kagera tarehe 17 Februari 2021, Dkt Mabula alisema ukosefu wa vifaa vya upimaji kwa halmashauri ni changamoto kubwa inayochangia kupunguza kasi ya upimaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kuwa, ununuzi wa vifaa vya upimani katika halmashauri siyo tu unaongeza kasi ya upimaji ardhi katika maeneo mbalimbali bali utasaidia kuongeza wigo wa mapato kwa kuwa maeneo mengi yatakuwa yamepimwa na kuingizwa katika mfumo wa kumbukumbu za ardhi.

Alizishauri halmashauri zinazonunua vifaa vya upimaji kuhakikisha vifaa hivyo vinatunza na kuhifadhiwa vizuri kutokana na kuwa na thamani na umhimu mkubwa katika suala zima la upimaji.

‘’Milioni 34 iliyonunua vifaa siyo fedha ndogo lazima anayehusika na kutunza vifaa awe makini na isije ikaonekana vifaa vimenunuliwa bila kutunzwa na nataka halmasahauri nyingine zione umuhimu wa kununua vifaa kwa kutumia fedha za ndani’’ alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, halmashauri zinazonunua vifaa vya upimaji zinaifanya Wizara kuangalia namna ya kuzisaidia katika zoezi zima la upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi na kusisitiza kuwa upimaji wowote unaofanyika unafuatiwa na umilikishaji.

Aidha, katika ziara yake, Dkt Mabula aligawa Hati za ardhi kwa wamiliki wa ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba ambapo aliwataka kuhakikisha wanalipia kodi ya pango la ardhi kwa wakati ili kuepuka kulimbikiza madeni ya kodi hiyo ambayo mwisho wa siku wataitwa wadaiwa sugu.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za mkoa wa Kagera kuzingatia sheria wakati wa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuwachukulia hatua wamiliki wanaoshindwa kulipa kodi ya pango la ardhi hata pale wanapopelekewa ilani za madai.