Ghana imekuwa nchi ya kwanza kupokea chanjo ya Covid-19 kutoka Covax, mpango wa ulimwengu wa kununua na kusambaza chanjo hiyo bure. 

Mpango wa Covax uliozinduliwa Aprili iliyopita kusaidia kuhakikisha usawa katika usambazaji wa chanjo ya virusi vya corona baina ya mataifa tajiri na masikini, umesema utakuwa imetoa dozi bilioni mbili kwa wanachama wake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. 

UNICEF, ambayo iliandaa usafirishaji wa chanjo hiyo kutoka Mumbai hadi mji mkuu wa Ghana, Accra, imesema katika taarifa ya pamoja na Shirika la Afya Ulimwenguni - WHO, kuwa wanayo furaha ya kufikisha chanjo za kwanza za Covid-19 chini ya mpango wa Covax. 

Katika taarifa hiyo, UNICEF imesema dozi 600,000 za chanjo ya AstraZeneca / Oxford yenye leseni kutoka kampuni yaa Serum ya India, ni sehemu ya kwanza ya shehena inayoelekea katika nchi kadhaa za kipato cha chini na cha kati.