Shirika la afya ulimwenguni WHO, limesema wafanyakazi wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamegundua kisa kipya cha virusi vya Ebola, ikiwa ni takribani miezi sita baada ya mlipuko huo kutangazwa kuwa umemalizika. 

Kisa hicho kimegunduliwa baada ya mwanamke mmoja aliyekuwa mke wa mtu aliyenusurika na ugonjwa wa Ebola, kutafuta matibabu katika kituo cha afya mjini Butembo mashariki mwa Congo ambako kulikuwa ni kitovu cha mlipuko. 

Mwanamke huyo alifariki baadae na majibu kuonyesha kuwa aliugua ugonjwa wa Ebola. Wafanyakazi wa afya wanaendelea kuwafuatilia zaidi ya watu 70 ambao wanaweza kuwa wamewasiliana na mwanamke huyo. 

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Congo ulidumu kwa karibu miaka miwili na kuwaua jumla ya watu 2,299 na wengine 1,162 walipona.