Na Mwandishi wetu, Moshi
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) Dkt. Yusuph Ngenya amewataka wajasiriamali wadogo wadogo nchini kuchangamkia fursa ya kupatiwa alama ya ubora bila malipo kwenye shirika hilo ili bidhaa zao zikubalike ndani na nje ya nchi.

Dkt Ngenya ameyasema hayo mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua mafunzo ya siku tano ya wazalishaji wa bidhaa mbalimbali.

Amesema wanavyo viwango vingi vya bidhaa za wajasiriamali wagodo hivyo wanawasaidia kuwapatia alama za ubora bila malipo kutokana na serikali kutenga fedha za kugharamia hayo.

“Wajasiriamali wadogo wadogo msiogope kuja kwetu TBS tuna mfumo wa kuwasaidia na nimesema hili mara nyingi kuwa wachangamkie fursa hii,” amesema Dkt Ngenya.

Ofisa mkuu wa viwango kutoka jumuiya ya Afrika Mashariki, Stella Apolot amesema kupitia mafunzo hayo yaliyoandaliwa kupitia EAC, GAZ na TBS wadau watatambua namna ya kufanya katika kuandaa bidhaa bora zaidi ya viwango.

Apolot amesema wadau hao wanapaswa kutambua kuwa utekelezaji wa viwango unapaswa kuwa rahisi kwa walaji na wasiwe watumiaji pekee.

Mwenyekiti wa kamati ya viwango wa TBS wa chuo kikuu cha Dar es salaam UDSM, Dkt Stephen Nyandoro amesema anatarajia washiriki watajifunza kuandaa na kuoanisha viwango mabalimbali katika nchi za Afrika Mashariki.

"Nchi nyingine za Afrika Mashariki hazipo vizuri kwenye biashara ya viungo ila kuna wenzetu wametoka Zanzibar wamebobea kwenye viungo na biashara ya viungo na baadhi ya maeneo ya Tanzania Bara," amesema Dk Nyandoro.

Mshiriki kutoka Zanzibar Khamis Issa Mohamed ambaye anasafirisha bidhaa za viungo kutoka Zanzibar kwenda Ulaya amesema utaratibu wa kuoanisha viwango ndani ya nchi za Afrika Mashariki utaongeza tija kwenye bidhaa zao.


Mohamed amesema baada ya mafunzo hayo watajenga uelewa mzuri zaidi na kuwekwa utaratibu wa viwango vinavyolingana.

"Unapokuwa unasafirisha bidhaa inapaswa kuwa na viwango vinavyotakiwa na kuwa balozi kwani unapofanya vizuri unaitangaza nchi ila ukipeleka bidhaa isiyo na viwango unaitukanisha nchi yako,” amesema.