TIGANYA VINCENT, RS TABORA
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania Jenerali Venance Mabeyo amevitaka vyombo vya ulinzi wa usalama kuendeleza mshikamano na ushirikiano uliopo ambao umesaidia kujenga imani kubwa kwa wananchi na kuimarisha ulinzi wa Nchi.

Alisema panapo kuwemo na mshikamano wananchi wanaona na wanakuwa na imani kubwa kwao na kuwaunga mkono.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Jenerali  Mabeyo alisema hayo leo alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora akiwa ziarani mkoani humo.

Alisema katika hali iliyopo ya sasa ulimwenguni vyombo vya ulinzi na usalama vinatakiwa kuwa na ushirikiano kwa ajili ya kukabiliana na mtu yoyote toka ndani na nje mwenye nia mbaya.

“Adui wa sasa anaweza asijitokeze mmoja kwa mmoja , bali anaweza kuwa miongoni mwenu…hivyo ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama ni jambo muhimu katika kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini”alisisitiza.

Jenerali Mabeyo aliwataka vyombo vya Ulinzi na Usalama waliopo katika ngazi za chini kuendelea kuimarisha ushirikiano kama wanavyofanya kwa ngazi ya Kitaifa.

Alisema kwa ngazi ya Taifa kila wakati wanashirikiana na wapo pamoja katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha Jenerali  Mabeyo amewashukuru wananchi wa Tanzania kwa utulivu wa hali ya juu waliouonyesha wakati zoezi la uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema hali ilitokana imani kubwa ambayo wananchi wanayo kwa vyombo vyao vya ulinzi na usalama katika kulinda amani na usalama wa Nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philemon Sengati alisema wameanzisha utaratibu wa kukutana kila mwisho mwezi kwa vyombo vote vya ulinzi na usalama mkoani humo kwa lengo la kujenga umoja.

Alisema kuwa katika kufakikisha hilo wanafanya mazoezi ya pamoja na kujadiliana ikiwa ni sehemu kuwa kitu kimoja.