Rais wa Marekani Joe Biden anasema hataondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran hadi itakapotimiza makubaliano yaliyofikiwa chini ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.
 

Biden alikuwa akizungumza na shirika la habari la Marekani CBS News la Marekani, kwenye mahojiano yaliyotangazwa Jumapili.

Lakini kiongozi wa ngazi ya juu zaidi wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema Tehran itarejea tu kwenye utekelezajiwa wa makubaliano hayo kama Marekani itaondoa kwanza vikwazo vya kiuchumi dhidi yake.

Mkataba wa mwaka 2015 ulilenga kuweka ukomo wa mpango wa nyuklia wa Iran, iwapo ingetaka kulegezwa kwa vikwazo hivyo.

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, hatahivyo, aliiondoa Marekani katika mkataba huo mwaka 2018 na kuiwekea tena vikwazo, na hivyo kuifanya Iran kuacha kutekeleza baadhi ya ahadi zake katika mkataba huo.

Iran, ambayo inasema kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani, imekuwa ikiendelea kuongeza kiwango chake cha ururubishaji wa madini ya uranium. Madini ya uranium yaliyorutubishwa yanaweza kutumiwa kutengeneza mabomu ya nyuklia.