Na Shamimu Nyaki – WHUSM,Dodoma
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Wizara inaendelea kusimamia  na kuratibu vyema shughuli za ubunifu kwa vijana kwa maslahi yao na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo Februari 04, 2021 alipokua akifungua Kongamano la I HAVE A DREAM  kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Mkoa wa Dodoma lililofanyika ukumbi wa Royal Village Jijini Dodoma  ikiwa ni kuelekea Tamasha la Serengeti Music Festival ambalo kilele chake ni Fabruari 06, 2021 Uwanja wa Jamhuri jijini hapo.

"Wizara inaweka mazingira mazuri kwa wabunifu ili waweze kufanya kazi za ubunifu katika maeneo waliyopo na kutimiza ndoto zao" alisema Mhe. Bashungwa.

Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa lengo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, la kuihamisha Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kwenda Wizara hiyo ni ili isimamie vyema kazi za wasanii ambao ndio wadau wakubwa.

"Kila mtu ana ndoto ambayo anatakiwa aitimize katika umri alionao na umri ujao auwekee malengo ya kuendeleza ndoto hiyo " Mhe. Bashungwa.

Mhe. Bashungwa ameongeza kuwa kila mtu yupo duniani kwa ajili ya jambo fulani hivyo ni vizuri kila mtu akawajibika katika kufanikisha jambo hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira) Mhe. Patrobas Katambi akitoa mada katika Kongamano hilo amesema kuwa hakuna kitu kigumu kinachorudisha nyuma mafanikio kama kuwa na woga na hofu, hivyo lazima vijana watambue hilo.

"Simama katikati ya watu wote ili wakuone una nini cha tofauti na wao na uonyeshe kwa vitendo kitu hicho" alisema Mhe. Katambi.

Naye Mhe. Erick Shigongo Mbunge wa Bichosa amesema kuwa safari ya mafanikio inaanza kidogo kidogo kwa kujifunza kila kitu bila kukata tamaa na hatimaye kupata   mafanikio binafsi hatimaye kwa Taifa, ambapo amewasihi vijana kuwajibika katika kutimiza malengo yao.

Vile vile Msanii na Mjasiriamali Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole amewashauri vijana kutumia muda vizuri katika kubadili maisha yao, huku msanii Kala Jeremia akisisitiza kuwa kila ndoto lazima iambatane na malengo.