Wizara ya Kilimo nchini  imesema malipo ya mazao yanayouzwa kwenye minada ya ushirika  yanatakiwa kufanyika ndani ya saa 72.

Naibu Waziri wa Kilimo,   Hussein Bashe amelieleza Bunge leo Jumatano Februari 10, 2021  kuwa malipo hayo ni sheria kwamba mkulima anatakiwa kupewa pesa zake kwa muda huo.

Kulingana na maelezo ya Bashe,  mkulima anatakiwa kulipwa fedha zake ndani ya siku tatu tangu mnada wa mazao husika utakapofanyika.

Naibu waziri huyo ameeleza hayo wakati akijibu  swali la mbunge wa Viti Maalum,   Sophia Mwakagenda  aliyetaka kujua utaratibu wa malipo kwa mazao ya wakulima wanapouza kwenye minada ya mazao kupitia vyama vya ushirika.

Hata hivyo,  Bashe amesema ulipaji kwa zao la cocoa ni tofauti kwani mkulima hulipwa fedha tangulizi kabla ya kuuzwa na baada ya kuuzwa anaongezewa  kiasi kilichozidi.

Ametaja sababu ya kuwa na utaratibu tofauti kwa zao la cocoa ni kwa sababu mazao hayo yanalimwa kwenye majumba ya watu na uvunaji wake ni kidogo kidogo.